Mfahamu Zion Clark: Mwanaume Asiye Na Miguu Aliyeweka Rekodi Ya Kutembea Kwa Kasi Zaidi Duniani
Zion Clark
Watu wengi huamini kwamba mtoto akizaliwa na ulemavu, basi hawezi kuwa na uwezo wowote wa kufanya mambo makubwa maishani mwake na wengi huchukuliwa kama mizigo, huku jamii nyingine zikiwa na imani potofu kwamba kuzaa mtoto mwenye ulemavu ni laana.
Hata hivyo, Zion Clark aliyezaliwa bila miguu, ameuthibitishia ulimwengu kwamba kuzaliwa na ulemavu siyo kikwazo kabisa katika maisha na kuonesha kwamba kumbe hata walemavu, wanaweza kufanya mambo makubwa na kuweka rekodi ambazo haziwezi kusahaulika duniani.
Zion mwenye umri wa miaka 24 ameingia katika kitabu cha rekodi duniani cha Guiness World Record na hii ni baada ya kufanikiwa kutembea kwa kutumia mikono yake kwa umbali wa mita ishirini kwa muda wa sekunde 4.7 na kuweka rekodi ya mtu asiye na miguu mwenye kasi zaidi duniani.
Kijana huyo ambaye ni mzaliwa wa Ohio, Marekani, alizaliwa bila miguu na pia akabainika kuwa na tatizo ambalo kitaalamu huitwa caudal regressive syndrome, ambalo husababisha maeneo ya chini ya kiuno kushindwa kukua kama binadamu wengine.
Rekodi hiyo ya Zion, imewashtua watu wengi duniani kote kwa sababu haijawahi kuwekwa na mtu yeyote kabla yake na sasa anatazamwa kama mfano wa jinsi ulemavu usivyoweza kuwa kikwazo katika maisha ya binadamu hapa duniani.
Licha ya kuzaliwa na ulemavu, Zion alionesha mapenzi makubwa kwenye michezo mbalimbali tangu akiwa mdogo na akiwa shuleni katika Shule ya Massillon, Ohio nchini Marekani, alikuwa akishiriki kwenye mchezo maarufu nchini Marekani wa miereka pamoja na michezo mingine na kupata umaarufu mkubwa.
Zion alizaliwa Septemba 29, 1997 katika Mji wa Columbus, Ohio nchini Marekani. Kama ilivyoelezwa, alizaliwa akiwa tofauti na watoto wengine kwani hakuwa na miguu na baadaye, akaja kubainika kuwa na tatizo la Caudal Regression Syndrome.
Inaelezwa kwamba hali aliyokuwa nayo, ilisababishwa na mama yake mzazi ambaye alikuwa na tatizo la matumizi ya madawa ya kulevya, hali inayotajwa kuwa ndiyo sababu ya kumzaa Zion akiwa na ulemavu.
Matumizi ya madawa ya kulevya na umaskini wa mwanamke huyo, ulimfanya ashindwe kumlea mwanaye huyo ambaye alipelekwa kwenye kituo cha kulelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Maisha katika kituo hicho, hayakuwa mepesi, mara kwa mara watoto wenzake walikuwa wakimfanyia vitendo vya unyanyasaji, kumpiga na kumjeruhi kwa sababu ya ulemavu wake lakini mwenyewe anaeleza kwamba tumaini lake lilikuwa kwa Mungu wake.
Baadaye, aliasiliwa na familia ya mwanamke mmoja wa Kimarekani ambaye hakubahatika kupata mtoto wa kumzaa na hapo ndipo maisha yake yalipoanza kubadilika, kwani alipelekwa kwenye shule nzuri na kuanza kupata matunzo yote muhimu. Akiwa anasoma katika shule ya Massillon High School, Zion alikutana na kocha Gil Donahue ambaye alivutiwa na jinsi alivyokuwa anapenda michezo licha ya ulemavu wake na akaahidi kumsaidia.
Miaka michache baadaye, akiwa chini ya usimamizi wa kocha huyo, Zion tayari alishakuwa miongoni mwa wacheza miereka wakubwa shuleni hapo, akiwashangaza wengi kwani alikuwa na uwezo wa kushindana na wanafunzi wenzake ambao hawana ulemavu wowote na kuwashinda.
Aliendelea kuwekeza nguvu kubwa kwenye mchezo wa miereka na baadaye akaja kushiriki kwenye mashindano makubwa ya wanafunzi ya miereka jimboni Ohio, maarufu kama D-I Ohio High School State Wrestling Championships ambako nako aliendelea kuonesha uwezo mkubwa na kuwashangaza wengi.
Baadaye, Zion alijifunza pia mchezo mwingine, riadha kwa watu wenye ulemavu ambapo alikuwa akikimbia kwa kutumia kiti maalum chenye magurudumu, huko nako akawa anaonesha uwezo mkubwa siku hadi siku na baadaye akaja kushinda katika mashindano makubwa ya jimbo hilo akiwa mshindi wa kwanza wa riadha kwa walemavu.
Kipaji kikubwa alichokuwa nacho, kikawavutia waongoza filamu wa Hollywood ambao walimuandalia ‘documentary’ ya maisha yake, iliyopewa jina la Zion ambayo kwa sasa inapatikana kwenye Netflix. Filamu hiyo ilipotoka kwa mara ya kwanza na kuoneshwa katika Maonesho ya Filamu ya Sundance Film Festival (2018) iliwashangaza wengi mno kutokana na kipaji kikubwa alichokuwa nacho na hapo sasa jina lake likaanza kuwa maarufu duniani kote.
Hakuishia hapo, bado alikuwa na ndoto kubwa ndani ya kichwa chake kwenye michezo na kwa mara nyingine, jina lake liliingia kwenye vichwa vya habari wakati wa michuano ya Olympic iliyofanyika Tokyo, Japan mwaka 2020 ambapo alishiriki katika michezo miwili kwa mpigo, miereka na riadha kwa walemavu kwa upande wa Paralympic.
Kwa sasa, Zion amejiunga na Chuo Kikuu cha Kent State ambako anaendelea na masomo yake ya digrii, huku pia akiendelea na mafunzo ya mchezo wa miereka kwa lengo la kufikia umahiri wa juu lakini pia akiendelea kujinoa kwenye michezo mingine mbalimbali ikiwemo kuinua vitu vizito na sarakasi.
No comments