Kocha Kipanga aipa Yanga faili la waarabu, Hersin atia neno
RATIBA ya Kombe la Shirikisho Afrika imetoka juzi mchana na Yanga imepangwa kuanza na Club Africain ya Tunisia, lakini Kocha wa Kipanga FC ya Zanzibar, Hassan Abdulrahman amewapa faili zima ili watinge makundi.
Kipanga ilikutana na Club Africain katika mechi mbili za hatua ya mtoano kabla ya kukutana na nyumbani walilazimishwa suluhu kabla ya kupoteza vibaya kwa mabao 7-0 ugenini nchini Tunisia.
Akizungumza na Mwanaspoti, Abdulrahman alisema wapinzani hao wa Yanga sio timu ngumu sana ingawa ina ubora wake ambao kikosi cha Kocha Nasreddine Nabi wanatakiwa kujipanga nao.
Alisema timu hiyo ambayo inatumia mfumo wa 3-5-2 ni timu ambayo Yanga inaweza kupata matokeo kulingana na ubora wa kikosi chao na ubora wao mkubwa upo kwa wachezaji wa eneo la kiungo na mabeki wa pembeni.
“Wanatumia mfumo wa 3-5-2 mechi zote mbili wametumia mfumo huo dhidi yetu kuna makosa tuliyafanya hasa mchezo wa ugenini lakini Yanga kwa timu waliyonayo wanatakiwa kutulia na kujipanga, wana nafasi ya kuwatoa, wanaweza kushinda hata mechi zote mbili,” alisema Abdulrahman na kuongeza;
“Tulipokutana nao kwao kuna wachezaji wao bora waliingia kipindi cha pili, hao ndio walikuja kutusababishia madhara, sio timu mbaya sana ila inawezekana ikatolewa.”
Kocha huyo aliongeza Yanga inatakiwa kujipanga na vurugu za mashabiki wa Club Africain ambao wanasafiri kwa wingi kuja hata ugenini ingawa huwa wanaigeuka timu yao inapocheza vibaya.
“Wanapocheza ugenini huwa wanafunguka sana kwa kushambulia kuliko wanapocheza nyumbani, nadhani kule wanahofia vurugu za mashabiki wao.
“Kama Yanga wakicheza vizuri kule ugenini wajiandae na vurugu za mashabiki wao huwa wanakuwa wakali kwa timu yao wanapoona mgeni anatawala mchezo, wale mashabiki wao sio kule au hapa, huwa hawaogopi Polisi kabisa.
“Kingine hawa jamaa hawakutufanyia uungwana tulipofika ugenini walitunyima kufanya mazoezi katika uwanja wa mchezo, sijajua kama na Yanga watawafanyia hivyo, walitupeleka hadi uwanjani wakatuambia tuuangalie tu uwanja lakini hatutafanyia mazoezi hapo na uwanja wao ni wa nyasi za kawaida kama vile Uwanja wa Mkapa.”
HERSI ATIA NENO
Wakati kocha wa Kipanga akiyasema hayo Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said alisema wameiona ratiba hiyo na baada ya hapo watakutana na makocha wao kisha kujipanga vizuri.
“Tumeiona ratiba kama mbavyo na nyie mmeiona, kilichopo mbele sasa ni kujipanga vizuri, tutakuwa na kikao na makocha wetu na kujiandaa kwa mechi hizo,” alisema Hersi kwa ufupi.
No comments