Ukweli tamu na chungu kuhusu Yanga, ripoti kamili iko hivi

TANZANIA imebakia na wawakilishi wawili tu katika mashindano ya Klabu Afrika ambao ni klabu za Simba na Yanga.
Simba wameendelea kupeperusha bendera ya Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kutinga kibabe hatua ya makundi baada ya kuitupa nje Primeiro de Agosto ya Angola kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-1.
Kwa upande wa Yanga wao wametolewa kwenye Ligi ya Mabingwa na Al Hilal ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-1 na kuangukia katika hatua ya mchujo ya Kombe la Shirikisho.
Simba kufuzu makundi kwa rekodi nzuri ya kushinda mechi zote nne nyumbani na ugenini, ni muendelezo wa kufanya vizuri kwenye mashindano hayo makubwa kila wanaposhiriki kulinganisha na klabu nyingine ikiwemo Yanga. Historia inaonyesha kuwa licha ya Yanga kutwaa mataji mengi ya Ligi Kuu Bara imekuwa haifanyi vizuri mara kwa mara kimataifa.
Tangu mashindano ya klabu Afrika yalipobadilishwa 1998, Simba ndio klabu ya Tanzania ambayo imefanya vizuri zaidi kuliko nyingine. Licha ya Yanga kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika tangu ilipoanza rasmi mwaka 1998, haijafanya hivyo tena kwa miaka 23 hadi sasa ingawa ilitinga katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mara mbili ambazo ni 2016 na 2018.
Simba kuanzia mwaka huo 1998 hadi sasa, wameingia hatua ya makundi mara tano tofauti ambapo mara nne ni katika Ligi ya Mabingwa Afrika na mara moja katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Kati ya mara hizo tano walizotinga hatua ya makundi, mara tatu tofauti walisogea hadi robo fainali na iwapo safari hii watasogea tena itakuwa ni mara ya nne. Nyuma ya kufanikiwa kwa Simba kimataifa kuna ukweli mchungu ambao lazima umefafanuliwa na wadau mbalimbali wametia neno. Twende pamoja;
Mahusiano mazuri kimataifa
Baada ya kukumbana na vipigo vya aibu misimu ya awali, Simba waliamua kuungana na wapinzani wao kutoka Uarabuni. Lengo lilikuwa ni moja tu. Kujifunza wanakosea wapi? Hapo wakaanza kujipambanua kama timu yenye mtandao mkubwa wa mahusiano na taasisi tofauti za kisoka nje ya nchi kuanzia klabu hadi mashirikisho pendwa duniani.
Mahusiano hayo kwa kiasi kikubwa yameimarishwa tangu ilipoanza kuwa chini ya bilionea Mohammed Dewji ‘MO Dewji’ akishirikiana na wanachama waandamizi wa Simba maarufu kama Friends of Simba. Ilianza kufanya ziara kubwa za ndani na nje ya Afrika ambazo zilifungua milango mbalimbali ya fursa kwa klabu hiyo huku ikipata fursa ya kujifunza mengi ya ndani na nje ya uwanja.
Dewji mwenyewe alifanya ziara hadi Fifa na Caf na kupata fursa ya kukutana na viongozi mbalimbali.
Alikutana na Rais wa Caf, Patrice Motsepe ambaye pia ni mfanyabiashara mkubwa kama yeye na mtu mzito kwenye soka la Afrika. Ukiondoa Dewji, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Mulamu Nghambi na Mtendaji Mkuu wa Klabu hiyo, Barbara Gonzalez kwa nyakati tofauti walifanya ziara ya kikazi katika klabu za Zamalek na Al Ahly za Misri. Walienda pia Morocco wakajenga urafiki na Berkane.
Kupitia ziara hizo za miaka tofauti, Simba ilipata darasa kwa kufahamu nini ambacho kinachangia mafanikio ya taasisi hizo, elimu ambayo walianza kuitumia na sasa inaanza kuwatofautisha na klabu zingine.
Kwenye ufundi, Simba wamejifunza namna gani ya kufanya usajili unaoendana na mahitaji ya mashindano hayo baada ya awali kujikwaa misimu kadhaa walipokuwa wakifungwa idadi kubwa ya mabao. Walijifunza namna usajili unavyofanyika na timu zinavyoandaliwa.
BAJETI, MIPANGO
Fungu la fedha ambalo Simba imetenga kwa ajili ya mechi za kimataifa ni ishara tosha ya namna uongozi wa Simba unavyoyapa uzito na thamani kubwa mashindano ya klabu Afrika kulinganisha na watani zao Yanga ambao wamewekeza zaidi kwenye ligi ya ndani.
Fedha hizo ni zile zinazotumika katika kuisafirisha timu pamoja na huduma za malazi, chakula na posho lakini pia kuna bonasi kubwa ya fedha ambayo imetenga kwa mechi za nyumbani na ugenini.
Kwa upande wa bonasi, Simba imeweka utaratibu wa kutoa kiasi cha Sh 100 milioni za bonasi iwapo timu inapata ushindi kwa mechi ya nyumbani ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Sh 50 milioni kwa Kombe la Shirikisho Afrika.
Ushindi wa mechi za ugenini za Ligi ya Mabingwa Afrika, unafanya nyota wa Simba kuvuna kitita cha Sh 200 milioni wakati zile za Kombe la Shirikisho Afrika wanapata kiasi cha Sh 100 milioni.
KWA MKAPA
Simba inafahamu kutumia vyema Uwanja wa nyumbani wa Benjamin Mkapa kuliko Yanga na timu nyinginezo. Ndio walioupa umaarufu msemo wa “kila mtu ashinde zake” jambo ambalo limekuwa likizipa hofu timu pinzani na kuongeza kujiamini na morali kwa wachezaji wake. Uthibitisho wa hilo unaweza kuonekana kupitia takwimu za mechi 20 zilizopita za mashindano ya Klabu Afrika ambazo Simba na Yanga kila moja imecheza katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ambazo zinaonyesha kuwa Simba imefanya vizuri zaidi huku Yanga ikiwa na matokeo ya wastani.
Yanga imeshinda michezo nane kati ya 20 iliyopita ya Klabu Afrika iliyocheza katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, imetoka sare nane na imepoteza michezo minne.
Simba, katika mechi zao 20 zilizopita za kimataifa Kwa Mkapa, wameibuka na ushindi mara 16, wametoka sare tatu na wamepoteza mchezo mmoja tu.
UGENINI, MISRI
Uchunguzi wa miaka ya hivi karibuni umebaini kwamba Simba hawategemei mwaliko wa CAF kuwepo Misri kwenye siku muhimu ikiwemo ile ya kupanga ratiba yoyote ile inayowahusu. Simba imekuwa ikituma muwakilishi kwenye matukio hayo ikiwemo na yale mengine yanayohusisha klabu za Afrika ili kuwa karibu zaidi na viongozi waandamizi pamoja na klabu kubwa za Arabuni ambazo ni washindani wake.
Kupitia mtandao huo,wana ufahamu mkubwa wa mazingira tofauti ya soka la Afrika na yale ya Kijiografia pamoja na kijamii hivyo inakuwa rahisi kwao kujua ni wakati na mazingira gani wanatakiwa wafanye nini.
Simba wameweka utaratibu wa kutuma timu ya awali kwenda katika kila nchi ambayo kuna timu wamepangwa kukutana nayo katika mashindano hayo, ambayo huipa taarifa nyingi wanazozitumia kurahisisha kuisafirisha timu kwenda mahali husika.
MAONI YA WADAU
Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema; “Viongozi wa Simba wanaishi kwa malengo kwa maana ya mpira wameufanya biashara kwa sababu wameonja matunda yaliyopo hususani kuuza wachezaji kwa fedha kubwa kama waliyofanya kwa Luis Miquissone wakati anajiunga na Al Ahly.”
Kipa wa zamani wa Yanga, Benjamin Haule alisema; “Yanga ni timu nzuri lakini inashindana na nani? ukiangalia wengine wanapofanikiwa ni umoja uliopo miongoni mwao, wanashirikiana kwenye kila jambo tofauti na Yanga ambao ni mtu mmoja mmoja.” alisema Haule.
Aliongeza jambo lingine ni Yanga kushindwa kutumia uwanja wa nyumbani vizuri kimataifa.
Post Comment
No comments